TAMWA YATOA TAKWIMU YA TATIZO LA MIMBA ZA UTOTONI
Na Mwandishi wetu
Kila kukicha kumekuwa na kesi za migogoro ya ardhi, mirathi na hata kesi za wazazi kuozesha watoto wao yaani mimba za utotoni na ndoa za utotoni na hii ni changamoto kubwa inayoikabili nchi kwa sasa.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Chama cha waandishi wa habari wanawake (TAMWA) umeonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2012/2013 jumla ya matukio 228 ya mimba na matukio 42 ya ndoa za utotoni yaliripotiwa
Hata hivyo, mimba na ndoa za utotoni zimetajwa kuwa ni miongoni mwa vikwazo vinavyowapata watoto wa kike kwamba tatizo hilo bado ni kubwa kwa baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara na Visiwani.
Wakati Tanzania Visiwani hali ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikionekana zaidi katika Mkoa wa Kusini Pemba na Wilaya ya Kati Unguja, upande wa Tanzania bara maeneo yenye ukatili dhidi ya wanawake pamoja na mimba za utotoni yanaonekana katika wilaya za Kahama, Tarime, Sengerema, Newala, Mbulu, Bunda, Nkasi, Babati, Chunya, Dodoma, Bariadi, Busega na Singida vijijini.
Bokhe Odhiambo (31), mkazi wa Tarime mkoani Mara, anasema vitendo vya ukatilli dhidi ya wanawake ndani ya ndoa na mimba za utoto kwa watoto wa kike ni mambo ya kawaida na jamii wala haina muda wa kuyakemea.
“Kupigwa au kufanyiwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ndani ya ndoa, migogoro ya ardhi na mimba za utotoni kwa watoto wa kike ni mambo ya kawaida tu kwenye jamii yetu licha ya wasaidizi wa kisheria kutoa elimu,” alisema Odhiambo.
Kutokana na changamoto hiyo, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) kimejitosa kutoa msaada wa kisheria katika mikoa yenye changamoto lengo likiwa ni kupunguza tatizo hilo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), Aisha Bade anasema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo chama chake kimeamua kusambaza wasaidizi wa kisheria 400 nchi nzima lengo likiwa ni kusaidia kutatua migogoro ya ardhi na mirathi.
Bade anasema Tawla imebaini kuwa mikoa ya Pwani na Morogoro, Mtwara, Lindi, Arusha , Tanga, Shinyanga, Manyara na Mwaza inaongoza kwa kuwa na migogoro ya mirathi, vitendo vya ukatili na kuozesha watoto katika ndoa za utotoni.
Anasema kuwa mbali na mikoa hiyo pia mikoa ya Tanga, Arusha, Dodoma inaongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi pamoja na mirathi na hivyo juhudi mbalimbali zinahitajika kukabiliana na tatizo hilo. “Tumesambaza wasaidizi wa kisheria 400 nchi nzima lengo ni kutatua migogoro iliyopo hasa katika maeneo ya vijijini ambayo tumeona hayana msaada wa kisheria” anasema Bade.
“Mbali na mikoa hiyo pia mikoa ya Tanga, Arusha, Dodoma nayo ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwa na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi na miradhi na kwamba juhudi za pamoja zinahitajika kushirikia katika kutatua changamoto hiyo ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea kutokana na tatizo hilo”anasema Beda.
Anasema TAWLA ilianza mafunzo ya wasaidizi wa sheria mwaka 2006 na kutokana mafunzo hayo zaidi ya wananchi 4,600 wamenufaika kwa kupata msaada wa kisheria vijijini katika kipindi cha mwaka jana pekee.
No comments:
Post a Comment