UMOJA wa Ulaya (EU) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Plan umeanza mradi maalumu wa miaka miwili katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, kuzuia ndoa za utotoni na vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike utakaogharimu zaidi ya Euro 400,000.
Mradi huo utakaotekelezwa pamoja na shirika la utu wa mtoto (CDF) ambalo litafanya kazi moja kwa moja kwa wananchi utafanyika katika kata tano zenye vijiji 21.
Hafla ya kutia saini makubaliano ya kuanza mradi huo yalifanyika jana katika Ofisi za Umoja wa Ulaya baina ya Mkuu wa Ujumbe wa Ulaya Tanzania, Balozi Filiberto Sebregond na Mkurugenzi Mkazi wa shirika la Plan, Jorgen Haldorsen na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa CDF, Koshuma Mtengeti.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Sebregond alisema usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake ni moja na shughuli zao za msingi ambapo wamewekeza zaidi ya Sh bilioni 14 katika miradi ya maendeleo kwa wanawake.
Naye Haldorsen alisema tatizo la ndoa za utotoni ni kubwa nchini ambapo kwa mujibu wa takwimu watoto 37 kati ya 100 nchini kila mwaka wanaolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18, hivyo kuwa katika hatari ya kupata virusi vya Ukimwi na vifo vitokanavyo na uzazi.
Alisema katika wilaya hiyo ya Tarime tatizo ni kubwa zaidi kwani watoto wa kike 55 kati ya 100 wanaoolewa ndoa za utotoni huku watoto wa kike 40 kati ya 100 wakitendewa vitendo vya kukeketwa.
No comments:
Post a Comment