Mkurugenzi-Mtendaji-Tamwa-Valerie-Msoka-akifafanua-jambo.
*Kila siku watoto wengi hupata ujauzito
Grace Gurisha
TANZANIA ni miongozi mwa nchi za Afrika zenye idadi kubwa ya ndoa za
utotoni, hali inayosababisha mtoto wa kike kutokuwa na maendeleo.
Mkoa wa Shinyanga ulio kaskazini magharibi mwa Tanzania ndiyo
unaotajwa kuongoza kwa mimba na ndoa za utotoni, ikilinganishwa na mikoa
mingine.
Hali hiyo inasababishwa na mambo mengi yaliyowazunguka, jambo ambalo linamfanya mtoto wa kike kuishi katika mazingira magumu.
Mimba za utotoni zimekuwa zikiwatesa watoto katika baadhi ya mikoa
kutokana na watu kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na malezi ya
watoto na haki zao.
Ili kutokomeza ndoa hizi ni lazima watu wakaungana kwa pamoja kupiga vita ukatili huo, kwani mtoto wa kike ana haki ya kusoma.
Baadhi ya mila, desturi na sheria zinasababisha kuchangia ndoa za
utotoni kuongezeka kwa kasi kubwa, hali itakayomfanya mtoto huyo kuwa
mnyonge.
Vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti matukio ya kikatili kwa watoto
kwa uwazi na ukweli, hali inayofanya mtoto kuona kuwa anajaliwa.
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef)
zinaonesha kuwa, kwa siku moja, watoto 16 wanapata mimba za utotoni.
Hayo yanasemwa na Mkurugenzi Mtendaji Chama cha Wanahabari Wanawake
Tanzania (Tamwa), Valerie Msoka, baada ya kupokea tuzo ya CEFM Champion
kutoka kwa Balozi wa Canada nchini, Alexandre Leveque kuwa balozi wa
kupinga ndoa za utotoni na ukeketaji.
Msoka amekuwa mtu wa kwanza kutunukiwa tuzo hiyo, baada ya kuonekana
kuwa yeye ndiye anayefaha kuoneza elimu ya kutokomeza ukatili huo
kutokana na uhodari wake wa kupigania haki.
“Tuzo hii ni yetu wote, kama si kwa ushirikiano wenu wadau wa
maendeleo, vyombo vya habari ambavyo tumefanya kazi kwa karibu na jamii
kwa ujumla. Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kushikamana kuhakikisha
kuwa hadhi ya mtoto wa kike inalindwa ipasavyo,” anasema.
Anaongeza kuwa Canada ni nchi ambayo inapiga vita vitendo vya ukatili
kwa kijinsia hasa ndoa za utotoni kuhakikisha kuwa mtoto wa kike
anapata haki zake za msingi.
Anafafanua kuwa kampeni hiyo itakuwa endelevu kwa lengo la kuliweka
suala hilo lizungumzwe ili mtoto wa kike awe na haki sawa kama mtoto wa
kiume.
“Muacheni mtoto wa kike asome, acheze kama ni mtoto wa kiume, baadhi
ya watoto wamekuwa hawapati hata muda wa kucheza wao kazi yao kunisaidia
kazi za nyumbani na kuolewa.
“Hali inatisha kuna mtoto wa miaka 12 amefariki kwa sababu ya uzazi,
halafu mume wake yupo jambo linalotia simanzi mtoto anaangamia bila
hatia, tunatakiwa tuungane tutokomeze ukatili huu,” anasema Msoka.
Anasema ndoa za utotoni zinasababisha watoto kupata matatizo katika
njia yake ya haja ndogo wakati wa kujifungua, ambapo wengi wa watoto hao
wanapata fistula.
Pia, anasema mtoto akiozwa kwenye familia atateseka kwa sababu
atakuwa hana kauli ndani ya nyumba kutokana na mume wake kumdharau
kutokana na umri wake mdogo.
Anafafanua kuwa kinachotakiwa ni kuweka misimamo ya mambo mbalimbali
ili kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatoweka kwani kutokuweka msimamo
ni changamoto kubwa katika kampeni hii.
Anafafanua kuwa ukeketaji ni kitendo cha kuondoa au kukata kisehemu
au sehemu ya uke (kinembe) cha mwanamke kinachofanywa na mtu anayeitwa
ngariba.
Kitendo hicho kimekuwa na madhara kwa mtu anayefanyiwa ikiwemo
maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kutokana na kuchangia vifaa
vinavyotumika kukeketea.
Anasema madhara mengine ni kifo, ambapo kinasababishwa na kutoka damu
nyingi, hatari ya kupata maradhi na mwanamnke kupata maumivu makali
wakati wa kujifungua.
Balozi wa Canada
Balozi wa Canada
Kwa upande wa Balozi wa Canada nchini, Alexandre Leveque anasema
Msoka amekuwa mwanaharakati wa kwanza kutunikiwa tuzo hiyo na ubalozi
wake kama ishara ya kukubali mchango wake kupiga vita ndoa za utotoni na
ukeketaji kwa watoto wa kike.
“Msoka ametumia ujuzi wake kama mwanahabari aliyebobea, mwanaharakati
na mpenda maendeleo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali bila kujali
litakalomtokea au kueleweka vibaya na jamii ndiyo maana alistahili
kupata tuzo hiyo.
Balozi Leveque anasema watoto wa kike na wanawake wanafanyiwa vitendo
vya kiukatili, ambapo wanahitaji mtu wa kuwasemea: mtu ambae ataelezea
taarifa zao zinakazosaidia kuwaweka watu pamoja na kuleta mabadiliko
yenye tija, ambaye ni Msoka.
“Watoto wa kike milioni 14 duniani huozeshwa kila siku katika umri
mdogo chini ya 18 jambo ambalo ni kinyume cha haki za mtoto na ukiukwaji
wa haki za binadamu.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa ndoa za utotoni na
mikoa husika ni Shinyanga, Tabora, Mara, Lindi, Mbeya na Morogoro,”
anasema Balozi Leveque.
Pia, balozi huyo sanajari na hayo yote ameahidi kuunga mkono jitihada
zinazomlinda mtoto wa kike ili kuendeleza kampeni ya ‘Zero Marriage’
kwa mkoa wa Mara uliyozindiliwa mwaka 2014 na aliyekuwa mke wa Hayati
Nelson Mandela, Graca Machel.
Katibu Mkuu Maembe
Kwa upande Katibu Mkuu wa Wizara ya Jinsia na Watoto, Anna Maembe
ambaye na yeye alishuhudia kukabidhiwa kwa tuzo hiyo, ameiomba jamii
ibadili mtizamo wa katika masuala ya ndoa za utotoni wakati sheria ya
ndoa kwa watoto ikiwa bado inafanyiwa marekebisho katika mchakato wa
Katiba.
Anasema kuoa msichana au binti aliyechini ya umri wa miaka 18 ni ubakaji na kwamba mtoto si mke.
“Watoto wote ni wale walio na umri chini ya 18,lakini kutokana na
sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kutoa fursa kwa mtoto alie na miaka 14
kuolewa kunaleta tatizo kubwa kwa wadau wa kutetea haki za jinsia na
watoto.
Tunatambua hii sheria haitoi uhuru haki ya kupata elimu kwa mtoto
kike na Serikali ipo mbioni kuibadilisha lakini pia niiombe jamii kubali
mtizamo na asiwepo mtu anayekubali kukubali kumoza mwanaye angali akiwa
na umri mdogo,” anasema
Katibu huyo anasema utafiti unaonesha kwamba kati ya wasichana watano
wawili kati yao kupata mimba kabla ya kufikia umri wa miaka 18 kila
mwaka nchini Tanzania. Tunatakiwa tuungane kutokomeza ukatili huo.
No comments:
Post a Comment