Kila mwaka, watoto milioni 7.3 wa kike chini ya umri wa miaka 18
hushika na kujifungua mimba, imesema ripoti mpya kuhusu hali ya idadi ya
watu mwaka 2013, ambayo imetolewa na Shirika la Mfuko wa Idadi ya Watu
katika Umoja wa Mataifa, UNFPA. Taarifa kamili na Assumpta Massoi:
(RIPOTI YA CHANZO CHA HABARI)
Ripoti hiyo imesema, milioni mbili kati ya watoto hao milioni 7.3,
wana umri usozidi miaka 14, na kwamba watoto hao hukumbana na matatizo
ya muda mrefu ya kiafya na kijamii kutokana na mimba hizo, yakiwemo vifo
vinavyohusiana na uzazi.
Ripoti hiyo pia inatoa wito wa kubuni mbinu za kina za kukabiliana na changamoto za mimba za utotoni.
Inahimiza uwekezaji zaidi katika elimu ili kuhakikisha watoto wa kike
wanaendelea kuwa shuleni, kutokomeza ndoa za utotoni, kubadilisha
mitazamo kuhusu majukumu ya kijinsia na usawa wa kijinsia. Pia
inapendekeza kuongeza ufikishaji wa huduma za afya ya uzazi kwa watoto
walobalehe, zikiwemo kuzuia mimba na kuboresha usaidizi kwa wazazi wa
utotoni.
Alanna Armitage ni Mkurugenzi wa afisi ya UNFPA mjini Geneva:
"Mimba za utotoni huathiri afya, elimu na haki za mtoto wa kike.
Mtoto wa kike asiye na elimu atakuwa na ugumu kupata ajira na kujijengea
maisha bora na familia yake. Msichana anayeshika mimba akiwa na umri wa
miaka 14 au chini yake, haki zake zitakuwa zimekiukwa. Kuna wasichana
milioni 580 duniani sasa. Ripoti ya mwaka huu inaonyesha kuwa kwa
kuwekeza kwa watoto wa kike, kuwapa nguvu, na kulinda haki zao leo,
tunaweza kuwasaidia kufikia ndoto zao."
Ripoti hiyo inatoa mtazamo mpya kuhusu mimba za utotoni, ikiangazia
siyo tu tabia za watoto hao kama sababu za mimba hizo, bali pia vitendo
vya familia zao, jamii na serikali.
No comments:
Post a Comment