MOJA ya mambo yanayopigiwa kelele kila siku na serikali, wazazi,
wanaharakati na asasi za kiraia nchini ni mimba na ndoa za utotoni,
ambazo zimeshamiri katika baadhi ya mikoa hapa nchini.
Mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Kigoma na Tabora imetajwa kuwa kinara kwa
ndoa za utotoni, hali inayochangia ongezeko la mimba za utotoni.
Takwimu kutoka mashirika mbalimbali, likiwemo Shirika la Umoja wa
Mataifa Linaloshughulikia Watoto (UNICEF), zinaonesha kuwa kwa siku
watoto 16 wanapachikwa mimba za utotoni.
Aidha, utafiti uliofanywa hivi karibuni na Chama cha Waandishi wa
Habari Wanawake (TAMWA) umeonesha kuwa katika kipindi cha mwaka
2012/2013, jumla ya matukio 228 ya mimba na matukio 42 ya ndoa za
utotoni yaliripotiwa.
Pamoja na hayo, ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa
Linaloshughulika na Idadi ya Watu duniani (UNFPA) ya mwaka 2013,
ilibainisha kuwa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, kila siku
wasichana 20,000 walio chini ya miaka 18 hupata watoto huku vizazi tisa
kati ya 10 ya vizazi hivyo, vikitokea kwenye ndoa au mahusiano.
Kutokana na hali hiyo, idadi ya vizazi kwa wasichana walio chini ya
miaka 15, huenda ikaongezeka na kufikia milioni tatu kila mwaka ifikapo
mwaka 2030.
Matatizo hayo yalianza kuwa tishio tangu miaka ya nyuma, ambapo
utafiti kuhusu mimba za utotoni kwa wasichana uliofanywa mwaka 2010 na
TAMWA, ulitoa picha ya kutisha.
Mfano, mkoani Tabora pekee wasichana wa shule 819 walipata mimba
kipindi cha mwaka 2006-2009. Na Morogoro kati ya mwaka 2007-2009
wasichana wa shule 331 walipata mimba na kukatisha masomo yao.
Aidha, takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, zinaonesha
kuwa wasichana takribani 8,000 kila mwaka huacha shule kutokana na
ujauzito, ambapo kati ya hao 3,000 ni wanafunzi wa shule za msingi na
wanafunzi zaidi ya 5000 ni wa shule za sekondari.
Kama vile takwimu hizo hazitoshi kuonesha ukubwa wa matatizo hayo,
hivi karibuni mkoani Dodoma wazazi wenye mtoto wa kike mwenye umri wa
miaka 10, walilazimika kuburuzwa mahakamani kujibu mashtaka ya kumuoza
mtoto wao huyo kwa kijana wa miaka 25.
Tayari mtoto huyo alishalipiwa mahari ya mbuzi 12 na Sh 100,000 na
kijana aliyetaka kumuoa, anayefahamika kwa jina la Joshua Mnamba, ambaye
naye amefikishwa mahakamani tangu Februari 24, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, umri rasmi wa kufunga
ndoa kwa kijana wa kike ni kuanzia miaka 18, kinyume cha hapo ni sawa na
kumfanyia ubakaji mtoto atakayefunga ndoa chini ya umri huo.
Kukithiri kwa vitendo hivyo vya ndoa na mimba za utotoni ni wazi kuwa
kunasababisha watoto wengi wa kike, kukosa fursa ya kuendelea na masomo
na kulazimika kuwa na majukumu makubwa tofauti na umri wao.
Ukweli ni kwamba takwimu hizo zote, zinaonyesha kuwa bado kuna haja
kubwa ya kushughulikia tatizo hilo kuanzia ngazi ya chini ya wazazi na
walezi na hatimaye Serikali kwa ujumla ili kukomesha matatizo hayo
yanayowarudisha nyuma wasichana.
Iko haja mamlaka husika na asasi za kiraia, zinazoshughulikia masuala
ya haki za watoto, kuanza kuchukua hatua stahiki na kulichukulia suala
hilo kama janga la kitaifa, kutokana na ukweli kuwa takwimu hizo,
zinaonesha watoto wachache tu walioolewa au kupewa mimba na kubainika.
Adhabu kali zitolewe kwa wahusika, kuanzia wazazi au walezi
walioruhusu ndoa na mimba hizo, ikiwemo wanaume wanaooa na kuanikwa
hadharani ili iwe fundisho.
No comments:
Post a Comment